Rais Jakaya kikwete na Prince Aga Khan wakionesha Stampu mpya za posta walizozindua Ikulu jana.Stampu hizo zinaonesha mradi mbali mbali ya aga Khan ikiwa ni maadhimisho ya miaka 50 ya uongozi wake.
Na Mwandishi Maalum
RAIS Jakaya Kikwete amesema serikali yake na watanzania wanathamini michango na miradi mbalimbali ya kijamii ambayo Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Shia Ismailia Duniani, Mtukufu Karim Agha Khan amewekeza katika nchini.
Rais Kikwete aliyasema hayo juzi Ikulu wakati wa hafla ya chakula maalum ambacho Rais na Mama Salma, walikiaandaa kwa ajili kumpongeza kiongozi huyo kwa kusherehekea kutimiza miaka 50 ya uongozi wake.
Alisema watanzania wengi wamenufaika na miradi hiyo, ikiwamo ile ya elimu na afya na huduma nyinginezo.
Rais Kikwete alisema Watanzania wanajivunia ushirikiano mzuri ulipo kati yake na Kiongozi huyo, na akushukuru kwa kuichagua Tanzania kama moja ya nchi ya kusherehekea miaka 50 ya uongozi wake.
Akizungumzia ujenzi wa chuo hicho kikuu kipya mkoani Arusha ambako kiongozi huyo anatarajia kukijenga hivi karibuni, Rais Kikwete alisema serikali ina upokea na kuukaribisha uamuzi wake huo na kwamba itatoa ushirikiano wote ili kufanikisha utekelezaji wa maradi huo.
Akizungumza katika halfa hiyo, Mtukufu Karim Agha Khan, aliisifia serikali na Watanzania kuwa wanastahili pongezi kwa kuendeleza na kusimamia uhuru wa kuabudu kulingana na imani za kila mtu huku wakiishi kwa amani na utulivu.
Agha Khan alisema kutoka na Tanzania kuendeleza utamaduni huo wa wananchi wake kuishi na kushirikiana bila ya kujali tofauti zao za kidini, kunaifanya kuwa nchi ambayo ni kama zawadi kati ya nchi nyingine duniani.
?Licha ya kwamba idadi ya Wakristu na Waislamu ni karibu nusu kwa nusu, lakini mmendelea kuuenzi utamaduni huu wa kuishi kwa pamoja mkiheshimu imani za kila mtu, hili ni jambo ambalo serikali na Watanzania mnastahili pongezi kubwa,? alisema.
Alisisitiza kwamba, utaifa unaojengwa miongozi mwa Watanzania kwa kuishi kwa kuheshimiana bila ya kujali tofauti za kidini wala itikadi za kisiasa, ni msingi mzuri ambao Tanzania kama taifa, inajiwekea kwa siku za baadaye.
Pamoja na kupongeza namna Watanzania wanavyoishi bila ya kubaguana, Agha Khan pia alipongeza serikali na watu wake, kwa namna ambavyo wamekuwa wakipiga hatua mbalimbali za maendeleo.
Alisema licha ya kuambiwa na watu wake wa karibu, lakini hata yenye mwenye ameyashuhudia.
Miongoni mwa mafanikio ambayo alieleza, ni pamoja mageuzi ya kiuchumi na mwelekeo mzuri wa ukuaji wa uchumi na jitihada zinazofanywa na serikali katika kufanikisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia (MDGs).
Agha Khan alitaja mafanikio mengine ya Tanzania kuwa ni pamoja na uandikishwaji wa watoto wote wenye umri wa kwenda shule ambayo imefikia asilimia zaidi ya 90, utoaji wa chanjo mbalimabali kwa asilimia 80 kwa watoto chini ya miaka mitano na ukuaji wa uchumi kwa asilimia sita.
Akizungumzia zaidi kuhusu utekelezaji wa MDGs, alisema mafanikio yaliyopatikana katika kuhakikisha kwamba watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule wanapata fursa hiyo, kunaeleza changamoto ya kupanua na kuendeleza elimu ya sekondari.
Alisema ndiyo maana hata taasisi yake ya Agha Khan Foundation, imekuwa ikitilia mkazo katika uendelezaji na utoaji wa elimu, na kwamba atajenga chuo kikuu kipya nchini, ambacho kitakuwa ni mradi mkubwa kuwahi kijengwa na taasisi hiyo baadaya ya ule ambao umejengwa nchini Pakistani zaidi ya miaka 25 iliyopita.
Akifafanua zaidi kuhusu ujenzi wa chuo hicho, Agha Khani alisema kwamba ujenzi wa chuo kikuu hicho utakaofanyika Arusha, kitajenengwa kwa miaka 15 na kitagharimu dola za Marekani 450 milioni, ambacho kitakuwa na mchepuo wa sayasi na shule mbalimbali za kitaaluma.
Katika hatua nyingine, Kiongozi huyo mkuu wa madhehebu ya Shia Isimailia Dunian, pia amepongeza uhusiano mzuri uliopo katika ya serikali na sekta binafsi na kwamba ushirikiano huo ni muhimu katika ujenzi wa taifa.
Kabla ya hafla hiyo ya chakula maalum, Rais Kikwete, Agha Khan, walizindua stempu maalum ambazo zimetayarishwa na Shirika la Posta Tanzania (TPC), kama sehemu ya kusherehekea miaka 50.
Stempu hizo zinaelezea miradi mbalimbali ambayo kiongozi huyo amewekeza nchini Tanzania .