http://bcstimes.com/majira/viewnews.php?category=1&newsID=4674
Friday, March 18, 2005 -@0918 EAT (06:18 GMT)
Na John Daniel

Chuo Kikuu cha Aga Khan chaziduliwa Dar

Rais Benjamin Mkapa,akiweka tofali ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Aga khan, Barabara ya Sam Nujoma, Dar es Salaam jana. Anayeshuhudia ni Kiongozi wa Waislamu wa Madhehebu ya Ismailia duniani, Imam Karim Aga khan.(Picha na Richard Mwaikenda)

*Imam Aga Khan aahidi kutoa elimu bure

CHUO Kikuu cha Aga Khan, kinachotarajiwa kujengwa Dar es Salaam, kitatoa elimu bure kwa wasio na uwezo kifedha.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Kiongozi wa Waislamu wa Madhehebu ya Ismailia duniani, Imam Karim Aga Khan, wakati akimkaribisha Rais Benjamin Mkapa, kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo hicho Dar es Salaam.

"Pamoa na Chuo hiki kuwa cha kimataifa na kuwarahisishia Watanzania-, pia tutatoa udhamini wa bure kwa wanafunzi watakaokuwa na uwezo wa kusoma wasio na fedha,"alisema

Alisema Serikali pekee haiwezi kutosheleza mahitaji ya utoaji elimu, hivyo kuna kila sababu kwa taasisi za kidini na watu binafsi kushiriki kutoa elimu ili kuboresha maendeleo ya nchi husika

Alisema yeye na dini yake kwa ujumla wanafurahishwa na hali ya amani na utulivu uliopo nchini, hivyo kama Watanzania watapata elimu bora maendeleo ya Taifa yatarahisihwa zaidi.

Imam Aga Khan aliyefutana na mkewe Princes Zahra Aga Khan, alisema utoaji wa elimu katika chuo hicho itazingatia mitaala ya kimataifa.

Katika hotuba yake, Rais Mkapa alisema bila elimu ya kutosha Tanzania haina nafasi katika Jamii ya kimataifa.

"Katika dunia ya leo Tanzania bila elimu haina nafasi katika jamii za kimataifa, hatuwezi kukumbatia hali hiyo, badala yake kwa gharama zozote zile,"alisema Rais Mkapa na kuongeza.

"Njia pekee ya kujenga Afrika bora yenye ustawi ni elimu bora na ujuzi, nasema tunashukuru kutuletea msingi wa kutujengea uwezo," alisema.

Alisema taarifa ya Tume ya Afrika iliyoundwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, inaonesha tatizo kubwa la Bara la Afrika kwa ujumla ni elimu, hivyo ukombozi wake ni kuwapa Waafrika elimu ili bora.

Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na mabalozi wa nchi mbalimbali, Waziri wa Elimu na Utamaduni Bw. Joseph Mungai, Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Dkt. Pius Ng'wandu, na wakuu wengine wa Serikali na mashirika ya kimataifa.

Gharama za ujenzi wa Chuo hicho inakadiri kuwa ni zaidi ya dola za Marekani milioni 27 (sh. bilioni 27).