Free Media
http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/8/20/habari21.php
20/08/2007

Aga Khan asifu uvumilivu wa kidini nchini

na Mwandishi Maalum

KIONGOZI mkuu wa madhehebu ya Shia Ismailia duniani, Karim Aga Khan, amesema serikali na Watanzania wanastahili pongezi kwa kuendeleza na kusimamia uhuru wa watu kuabudu kulingana na imani zao huku wakiishi kwa amani na utulivu.

Aliyasema hayo wakati wa hafla ya chakula maalumu ambacho Rais Jakaya Kikwete na Mama Salma walikiandaa kwa ajili yake juzi usiku Ikulu, kumpongeza kwa kusherehekea miaka 50 ya uongozi wake.

Aga Khan alieleza kuwa, kuendelea kwa utamaduni wa wananchi kuishi na kushirikiana bila ya kujali tofauti zao za kidini, kunaifanya Tanzania kuwa nchi ambayo ni kama zawadi kati ya nchi nyingine duniani.

"Licha ya kwamba idadi ya Wakristu na Waislamu ni karibu nusu kwa nusu, lakini mmendelea kuuenzi utamaduni huu wa kuishi kwa pamoja mkiheshimu imani za kila mtu, hili ni jambo ambalo serikali na Watanzania mnastahili pongezi kubwa," alisema.

Alisisitiza kwamba utaifa unaojengwa miongozi mwa Watanzania kwa kuishi kwa kuheshimia bila ya kujali tofauti za kidini wala itikadi za kisiasa, ni msingi mzuri sana ambao Tanzania kama taifa inajiwekea kwa siku za baadaye.

Pamoja na kupongeza namna Watanzania wanavyoishi bila ya kubaguana, Aga Khan pia ameipongeza serikali na Watanzania, kwa namna ambavyo wamekuwa wakipiga hatua mbalimbali za kimaendeleo.

Alibainisha kwamba ndiyo maana hata taasisi yake ya Aga Khan Foundation, imekuwa ikitiliana mkazo katika uendelezaji na utoaji wa elimu, na ndio maana ameamua kujenga chuo kikuu kipya nchini Tanzania, chuo ambacho kitakuwa ni mradi mkubwa kuwahi kujengwa na taasisi hiyo baada ya ule ambao umejengwa nchini Pakistan zaidi ya miaka 25 uliyopita.

Akifafanua zaidi kuhusu ujenzi wa chuo hicho, Aga Khan, alibainisha kuwa ujenzi wa chuo kikuu hicho, kitakachojengwa Arusha, kitajengwa kwa miaka 15 na kitaghalimu dola za Marekani milioni 450.

Awali akimkaribisha katika hafla hiyo na kumpongeza kwa kutimiza miaka 50 ya uongozi wake, Rais Kikwete alisema serikali na Watanzania wanathamini michango mbalimbali ya kijamii ambayo kiongozi huyo amewekeza nchini.

Alisema Watanzania wengi wamenufaika na miradi hiyo ikiwamo ile ya elimu na afya na huduma nyinginezo.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa chuo kikuu kipya mkoani Arusha, Rais alisema serikali inaupokea na kuukaribisha uamuzi wake huo na kwamba itatoa ushirikiano wote ili kufanikisha utekelezaji wa maradi huo.